Beyonce amshinda Jay-Z tuzo za Grammy

NEW YORK: MWANAMUZIKI nyota Beyoncé Knowles mwenye miaka 43 amempita mumewe Shawn Corey Carter maarufu Jay-Z (54), baada ya kuweka historia ya kuwa msanii anayetajwa zaidi kwenye tuzo za Grammy ambapo tuzo za hivi karibuni ameingia katika vipengele 11.
Beyonce na Jay-Z walioana tangu mwaka 2008 ambapo walitajwa kwenye vipengele 88 kila mmoja, lakini Beyonce kwa sasa ameweka rekodi zaidi ya mumewe.
Beyonce ni miongoni mwa walioteuliwa katika vipengele vya Albamu Bora na Albamu Bora ya nyimbo za Country kupitia albamu ya ‘Cowboy Carter’ na Albamu ya ‘Texas Hold ‘Em’ inayotajwa kuwania tuzo ya Wimbo Bora wa Mwaka.
Beyonce hajawahi kushinda tuzo ya Albamu ya Mwaka, licha ya kuteuliwa katika kipengele hicho mara nne kwa tuzo zilizopita. Mwanzoni mwa mwaka huu, Jay-Z aliziponda Grammys kwa kumpuuza Beyonce katika tuzo hizo.
Nyota huyo wa rap amesema: “Sitaki kumwaibisha mwanadada huyu. Lakini ana Grammys nyingi kuliko kila mtu na hajawahi kushinda Albamu bora ya Mwaka.
Beyonce katika kinyang’anyiro hicho atakabiliana na wasanii Andre 3000, Sabrina Carpenter, Charli XCX, Jacob Collier, Billie Eilish, Chappell Roan na Taylor Swift ambaye ndiye mwanamke Tajiri zaidi kwa wanamuziki wa kike.
Kuteuliwa kwa Taylor katika kipengele cha Albamu bora kupitia Albamu ya ‘The Tortured Poets Department’ akiwa ameteuliwa mara sita kugombea tuzo hiyo.
Kwingineko, Charli, Billie, Kendrick Lamar na Post Malone wote wameteuliwa katika vipengele saba kila mmoja. Charli ambaye ametoa albamu yake ya ‘Brat’ mwezi Juni ameteuliwa katika vipengele vitatu.
Taylor, Sabrina na Chappell wote wameteuliwa mara sita kila mmoja, ikiwemo Albamu Ya Mwaka, Wimbo Bora wa Mwaka, Rekodi ya Mwaka na Msanii Bora Mpya.