Arsenal hawatanii msimu huu

LONDON: WASHIKA mitutu wa jiji la London Arsenal wameitandika Bayern Munich 3-1 na kupata ushindi wao wa kwanza dhidi ya miamba hiyo wa Ujerumani katika kipindi cha miaka 10, na kuendeleza rekodi yao ya ushindi wa asilimia 100 kwenye Ligi ya Mabingwa msimu huu, ushindi ambao umewaweka kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.
Jurrien Timber aliwaweka Arsenal mbele kwa bao la kichwa dakika ya 22 baada ya mpira wa kona, lakini kijana Lennart Karl aliisawazishia Bayern mabingwa mara sita wa Ulaya kabla ya mapumziko.

Arsenal walitawala kipindi cha pili na kuonesha upana wa kikosi chao, ambapo wachezaji wa akiba Noni Madueke na Gabriel Martinelli waliingia na kufunga mabao yaliyohitimisha ushindi wao wa tano katika michezo mitano.
Ilikuwa usiku tulivu kwa mshambuliaji hatari Harry Kane aliyerejea kaskazini mwa London, huku Bayern wakipokea kipigo chao cha kwanza msimu huu katika mashindano yote. Kwa matokeo ya Inter Milan kupoteza, Arsenal sasa ndiyo timu pekee yenye alama 15, na nafasi yao ya kufuzu hatua ya 16 bora inaonekana kuwa iko karibu sana.
“Tulienda ‘man to man’ kipindi cha pili na nafikiri leo tumekuwa bora sana, Kocha ni mwenye furaha sana. umekuwa usiku maalum sana kwetu.” – amesema Declan Rice, ambaye alifanya kazi kubwa katikati ya uwanja.

Zikiwa juu ya misimamo ya Ligi Kuu England na Bundesliga kwa tofaiti ya pointi sita kila moja, na zikiwa zimecheza bila makosa kwenye mechi zao nne za mwanzo za Ligi ya Mabingwa, Arsenal na Bayern zimekuwa timu bora zaidi Ulaya msimu huu.
Timu hizo zilikutana robo fainali miaka miwili iliyopita ambapo Bayern walikuwa vinara, lakini Arsenal wamefikia kiwango kipya tangu wakati huo na waliingia kwenye mchezo wa Jumatano wakiwa hawajapoteza michezo 15 mfululizo katika mashindano yote.




