Ancelotti aanza na sare Brazil

SAO PAULO: KOCHA mpya wa timu ya taifa ya Brazil Carlo Ancelotti ameiongoza timu hiyo katika sare ya 0-0 dhidi ya Ecuador usiku wa kuamkia leo Ijumaa katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia kwa bara la Amerika Kusini mchezo ambao kocha huyo wa zamani wa Real Madrid kwa mara ya kwanza alikalia benchi la ufundi.
Mechi hiyo ilijaa ufundi na mbinu za makocha huku ikiwa na nafasi chache sana kwa kila timu kuliona lango la timu pinzani huku kikosi cha timu ya taifa ya Brazil kikionekana kukosa ubunifu wa kuifungua safu ya ulinzi ya Ecuador.
AnceIotti alifanya mabadiliko mengi katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo ikilinganishwa na mtangulizi wake Dorival Júnior, aliyetimuliwa baada ya timu hiyo kufungwa 4-0 na Argentina. Mabadiliko hayo yaliisaidia Brazil kuwazuia wenyeji karibu mechi yote lakini ilishindwa kuwa wabunifu na kukosa makali katika kushambulia, dosari ambayo pia ilionekana chini ya watangulizi wa Ancelotti.
Kocha huyo wa Kiitaliano mwenye miaka 65 aliwapa nafasi wachezaji kama Vinicius Júnior na kumrudisha kiungo mkongwe Casemiro na mshambuliaji Richarlison kwenye kikosi cha kwanza, alimchezesha kwa mara ya kwanza beki Alex na kijana Estêvão kwenye winga ya kushoto kama mbadala wa Raphinha aanayetumikia adhabu.
Brazil ilionekana kujilinda dhidi ya Ecuador, ambayo haijapoteza mechi 14 zilizopita za nyumbani. Nafasi nzuri zaidi ya kikosi cha Ancelotti ilikuja dakika ya 22, wakati Vinicius Jr alipopiga shuti la karibu lililoishia mikononi mwa kipa wa Ecuador Gonzalo Valle.
Sare hiyo iliifanya Ecuador kujikita katika moja ya nafasi za kufuzu moja kwa moja za Kombe la Dunia kwa kuendelea kubaki nafasi ya pili na pointi 24. Brazil iko katika nafasi ya nne ikiwa na alama 22. Timu sita bora kutoka Amerika Kusini zitafuzu moja kwa moja Kombe la Dunia 2026 nchini Marekani, Canada na Mexico