Amorim ajibu kauli za Ronaldo

MANCHESTER: Kocha wa Manchester United, Ruben Amorim, ametoa majibu ya ukali kwa kauli za mkongwe wa klabu hiyo Cristiano Ronaldo, akisema ni wakati wa kuangalia mbele badala ya kubaki kwenye makosa ya zamani.
Ronaldo, aliyeshinda mataji manane akiwa na United, alimueleza mwanahabari gwiji Piers Morgan wiki hii kwamba Manchester United “iko kwenye njia isiyo sahihi” na kuongeza kuwa Amorim “hawezi kufanya miujiza” Old Trafford.
“Ureno tuna msemo sema, miujiza hutokea Fatima pekee (moja ya maeneo matakatifu ya hija za wakatoliki),” alisema nyota huyo wa Al-Nassr mwenye umri wa miaka 40, akilalamikia ukosefu wa dira ya muda mrefu ndani ya klabu hiyo.

Lakini Amorim, ambaye alichukua mikoba kutoka kwa Erik ten Hag mwezi Novemba mwaka 2024, alijibu kabla ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Tottenham Hotspur unaotarajiwa kupigwa kesho Jumamosi.
“Ni kweli, anayo heshima kubwa na maneno yake yana uzito, Lakini kinachotakiwa sasa ni kuangalia mbele. Tunajua tumefanya makosa mengi, lakini tunajaribu kubadilika. Tusiendelee kuzungumzia yaliyopita tuzingatie tunachofanya sasa.” – amesema Amorim
Kocha huyo Mreno amesema United inabadilisha mfumo wake wa ndani na mtazamo wa wachezaji, jambo lililosaidia kuleta mabadiliko uwanjani. United kwa sasa wanashika nafasi ya nane wakiwa pointi mbili pekee nyuma ya nafasi ya pili, baada ya mechi nne bila kupoteza. Huku akisema kutoshiriki mashindano ya Ulaya msimu huu kumewapa nafasi ya kujipanga upya.
“Wakati mwingine ni vizuri kuangalia faida kwenye changamoto Kama ningekuwa na nafasi ya kucheza Ulaya, ningeikubali. Lakini sasa tunapata muda zaidi wa kufundisha, kupanga na kuijenga timu upya.” aliongeza




