Mastaa

Aliyemuibia Kim Kardashian apanga kuomba msamaha

PARIS: MMOJA wa watuhumiwa katika kesi ya wizi wa kutumia silaha kwa mwanamitindo Kim Kardashian, Yunice Abbas, amesema anakusudia kuwajibika kwa kufanya uporaji mwaka 2016 na ataomba msamaha mahakamani kesi yao itakaposikilizwa huko Paris, Ufaransa.

Abbas, mwenye umri wa miaka 71, ambaye amekiri hadharani ushiriki wake katika wizi huo, ni miongoni mwa washukiwa 10 wanaokabiliwa na mashtaka ya utekaji nyara na wizi wa kutumia silaha.

“Nitaomba msamaha,” Abbas aliiambia Associated Press. “Namaanisha kwa dhati.”

Kim Kardashian mwenye miaka 44, anatarajiwa kutoa ushahidi wa moja kwa moja katika kesi hiyo Mei 23. Vito vyake vya thamani ya mamilioni ya dola viliibiwa katika ghorofa alipokuwa akiishi kwa Wiki ya Mitindo huko Paris nchini Ufaransa.

“Walifunga mkanda juu ya macho yangu na mdomo wangu, nilidhani waangenibaka na kuniua,” amesema Kardashian, akielezea wizi huo. “Lilikuwa jambo la kutisha zaidi ambalo nimewahi kupitia katika maisha yangu yote, nikifikiria tu kwamba, unakaribia kufa. Unajizatiti tu kwa wakati kwamba watakupiga risasi na kukuua. Dakika 10 hizo zilibadilisha maisha yangu yote.”

Mtuhumiwa wa tukio hilo alikamatwa Januari 2017 na amekaa gerezani miezi 21 kabla ya kuachiliwa chini ya uangalizi wa mahakama.

Katika akaunti yake, Kardashian ameeleza kwamba wanaume wawili walioingia kwa nguvu chumbani kwake na kumuelekezea bunduki, wakimuuliza ilipo pete yake.

Amesema alifungwa kwa nyaya za plastiki na mkanda huku wavamizi walichukua vito vyake vya thamani, ikiwa pamoja na pete yake ya uchumba yenye thamani ya mamilioni ya dola.

Related Articles

Back to top button