Alikiba: Mutimawangu yuko huru kufanya kazi na msanii yeyote

DAR ES SALAAM:MSANII wa Bongo Fleva, Ali Kiba, amesema msanii wake mpya, Mutimawangu, yuko huru kufanya kazi na msanii yeyote mwenye uwezo mzuri wa kuimba, ilimradi makubaliano yatakayofikiwa yawe na maslahi kwa pande zote. Amesisitiza kuwa lebo yake ya Kings Music haina mipaka ya ushirikiano, bali inalenga kukuza vipaji na kutoa uhuru wa ubunifu kwa wasanii wake.
Ali Kiba aliyasema hayo alipokuwa akimpokea Mutimawangu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, akitokea Kigali, Rwanda. Alieleza kuwa hakumchelewesha kwa bahati mbaya, bali alitaka kumpata msanii mwenye sauti ya kipekee, uwezo mkubwa wa kuimba na mvuto wa jukwaani.
“Kipaji chake kina sauti ya kipekee, ana muonekano mzuri na anajua kuimba vizuri sana. Anachotakiwa ni kuendelea kufanya muziki mzuri, kwa sababu kipaji kikubwa kinaweza kuuzwa popote,” amesema Ali Kiba, akiongeza kuwa hakumaanisha Tanzania haina wasanii wa kike wenye vipaji, bali Mutimawangu amebahatika kupata nafasi hiyo.
Alifafanua kuwa wasanii wa kike hukutana na changamoto nyingi zaidi ikiwemo masuala ya kihisia, mahusiano na maandalizi ya kazi, jambo linalohitaji muda na uvumilivu zaidi kutoka kwa menejimenti. Amesema lebo hulazimika kuzingatia afya, hali ya kihisia na mazingira ya kazi ili kumsaidia msanii wa kike kukua vizuri.
Ali Kiba amesema Mutimawangu amekaa muda mrefu akijifunza mambo mbalimbali kabla ya kuanza rasmi safari yake ya muziki nchini Tanzania, ikiwemo kujifunza Kiswahili na kuielewa tasnia ya Bongo Fleva, ili awe tayari kushiriki kikamilifu katika soko la muziki.




