EPLKwingineko

Arsenal yakubali kumsajili Rice kwa Bil 310/-

WASHIKA mtutu wa London, Arsenal imekubali dili lenye thamani ya pauni milioni 105 sawa na shilingi bilioni 310 kumsajili kiungo wa West Ham United ‘Hammers’, Declan Rice.

Mazungumzo yanaendelea kati ya klabu hizo kuhusu jinsi gani dili hilo litakavyotekelezwa kwa ajili ya kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24.

Hatua hiyo inafuatia ombi la tatu kutoka kwa Washika Mtutu hao ikiwa maombi mawili ya awali yalikataliwa baada ya kuwa pungufu ya pauni milioni 100 ilizotaka West Ham.

Mapema wiki hii, Manchester City ambayo ilikuwa na ofa ya pauni milioni 90 sawa na shilingi bilioni 265.9 iliyokataliwa ilijitoa kwenye kinyang’anyiro cha kumsajili Rice.

Nahodha huyo wa West Ham amekuwa kwenye klabu hiyo tangu ajiunge na shule ya soka ya Hammers akitokea Chelsea mwaka 2014.

Ombi la Arsenal linajumuisha pauni milioni 100 za awali pamoja na nyongeza ya pauni milioni 5.

Mapema mwezi huu Rice aliiongoza West Ham kutwaa Kombe la Ligi ya Europa Conference likiwa la kwanza kubwa kwa klabu hiyo katika muda wa miaka 43.

Mkataba wa Rice katika klabu ya West Ham unamalizika 2024.

Ada kubwa zaidi ya uhamisho kuwahi kutokea katika Ligi Kuu ya England ni pauni milioni 107 sawa na shilingi bilioni 316 Chelsea ilizoilipa Benfica kumsajili kiungo wa Argentina Enzo Fernandez Januari mwaka huu.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button