Enzo Fernandez avunja rekodi usajili England

KLABU ya Chelsea imemsajili kiungo wa Muajentina wa timu ya Benfica ya Ureno Enzo Fernandez kwa ada ya uhamisho iliyovunja rekodi England ya pauni milioni 107 sawa na shilingi bilioni 305.9.
Amesaini mkataba wa miaka minane na nusu kutumikia Stamford Bridge.
Mkataba huo unapita kiasi cha pauni milioni 100 sawa na shilingi bilioni 285.9 ambacho Manchester City ililipa kumsajili Jack Grealish mwaka 2021.
Fernandez ambaye alijiunga na Benfica kwa pauni milioni 10 sawa na shilingi 28.5 Agosti, 2022 alitangazwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi wakati michuano ya Kombe la Dunia iliyofanyika Qatar 2022 Argentina ikiibuka mabingwa.
Ripoti zinasema nyota huyo Muajentina yupo njiani kwenda London.
Kwa mujibu wa tovuti ya uhamisho wa wachezaji, Transfermarkt, usajili wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 kunaifanya Chelsea kuwa imetumia pauni milioni 289 sawa na shilingi bilioni 826 katika dirisha la Januari.
Fernandez, aliyesajiliwa Benfica kutoka River Plate ya Argentina, amefunga mabao manne katika michezo 29 akiwa timu hiyo ya Ligi Kuu ya Ureno.