Mastaa

Msimamizi wa gereza akanusha madai ya Tory Lanez

CALIFORNIA: MSIMAMIZI wa gereza, Thomas Valdez anayeshtakiwa na rapa Tory Lanez amepinga vikali kesi hiyo ya madai ya Dola milioni 100.

Nyaraka za mahakama zilizonaswa na Mtandao wa TMZ ambazo zimewasilishwa na Valdez, zinakanusha kuwa Tory alidhuriwa kutokana na hatua yoyote aliyochukua yeye na kupuuzia mbali madai kwamba haki za Tory zilivunjwa.

Aidha, Valdez amekiri Tory alichomwa kisu na mfungwa Santino Casio, kwa kutumia silaha iliyotengenezwa na wafungwa wenyewe, wakati wote wawili wakiwa katika kituo hicho.

Tory amedai kuwa hawakupaswa kuwekwa katika eneo moja kutokana na historia ya Casio ya vitendo vya vurugu.

Tory amefungua kesi dhidi ya Idara ya Marekebisho ya California, msimamizi wa gereza, na maofisa 50 wa magereza katika gereza hilo ambako anatumikia kifungo chake, akidai fidia ya kiasi hicho cha pesa.

Mei 12, mwaka jana, Tory alikimbizwa hospitalini baada ya kuchomwa kisu mara 14, na kupata majeraha yaliyoathiri mapafu yake.

Tory anawalaumu maofisa hao kwa tukio hilo, akidai kuwa hawakuwepo eneo la tukio kama ilivyopaswa kuwa. Anadai uongozi wa gereza ulikuwa na mtazamo wa kutojali kwa makusudi kuhusu vitendo vya vurugu ndani ya gereza hilo.

Related Articles

Back to top button