Kwingineko

Saido Berahino atundika daruga, ageukia ukocha

BUJUMBURA: ALIYEKUWA mshambuliaji wa timu ya taifa ya Burundi, Saido Berahino ametangaza kustaafu kucheza soka baada ya kudumu dimbani kwa miaka 15.

Nyota huyo wa zamani wa West Bromwich Albion ya England ameeleza kuachana na soka akiwa hana anachodai kutokana na manufaa aliyoyapata kupitia mchezo huo.

“Mpira wa miguu umenipa kila kitu. Kutoka mitaa ya Bujumbura hadi Hawthorns. Kutoka Ligi Kuu England hadi maeneo ambayo sikudhani ningecheza. Huu mchezo umembeba mtoto mdogo mkimbizi katika maisha.

“Napenda kuishukuru West Bromwich Albion kwa kuniamini wakati nilipokuwa mvulana. Miaka yote klabuni, mabao, mashabiki na nyakati, mara zote zitaendelea kuwa za kipekee.

“Kwa kila mchezaji mwenzangu, kocha na shabiki ambaye ameshiriki katika safari, asante sana,” amefafanua Berahino.

Berahino, 33 alihamia England akiwa na miaka 10 baada ya familia yake kupewa hifadhi ambapo alijiunga na Albino akiwa na miaka 12, kabla ya mwaka 2017 kuhamia Stoke City.

Baadaye alitimkia klabu ya Zulte Waregem ya Ubelgiji kabla ya kurejea England kukipiga Sheffield Wednesday msimu wa 2021-22 na kuwa timu ya mwisho kuitumikia England.

Mara ya mwisho mwaka jana, Berahino aliitumikia Tabor Sezana inayoshiriki Ligi Daraja la Pili Slovenia.

“Kulikuwepo upandaji na kushuka, makosa na mafunzo. Nimejifunza kwamba mchezo unaweza kukupandisha na kukupa kipimo muda huohuo. Katika yote hayo, soka lilibakia palepale kwangu.

“Muda umefika wa kuning’iniza viatu vyangu. Mwili wangu na moyo wangu vipo tayari kwa ukurasa mpya. Naona fahari na nashukuru kwa sasa kuiwakilisha timu ya taifa ya Burundi kama kocha.

“Hii sio kusema kwaheri kwa mpira wa miguu. Kirahisi tu hii ni mwisho wa hadithi moja na mwanzo wa nyingine. Kwa upendo na shukurani,” amesema Berahino.

Related Articles

Back to top button