Slot aendelea kukuna Kichwa Liverpool

LIVERPOOL: Mabingwa watetezi wa ligi kuu ya England Liverpool walilazimika kutegemea shuti la ‘deflection’ la Florian Wirtz lililojaa wavuni dakika ya 81 kujiokoa na kipigo na kupata sare ya 1-1 dhidi ya Sunderland kwenye mchezo wa ligi hiyo wa Jumatano usiku, mchezo uliotafsiriwa kama hatua moja nyuma baada ya awali kupata ushindi wa 2-0 walioupata dhidi ya West Ham United wikiendi iliyopita.
Bao hilo liliwaepusha Liverpool aibu ya kupoteza mechi ya 10 katika mechi zao 14 zilizopita kwenye mashindano yote, katika msimu ambao umekuwa safari ya hatua moja mbele na nyingi nyuma kwa kikosi cha Arne Slot.
“Mara nyingi sana msimu huu haturuhusu nafasi nyingi dhidi yetu, lakini chache zinazopatikana zinatuumiza. Hatukupata bahati ya kupata ushindi, lakini kwa hali tuliyokuwa nayo wiki za hivi karibuni tungepoteza mchezo huu hivyo kupata sare kuna kitu tumejifunza.” – Slot ameiambia BBC kwa sura iliyokosa furaha.
Hata hivyo, kocha huyo Mholanzi alikiri tatizo kubwa linaloendelea kukisumbua kikosi chake ni ubutu wa safu yake ya kushambulia.
“Tuko kwenye mechi ya 14 sasa lakini bado hatujaweza kufunga mabao ya kutosha kutokana na ‘open play’ au mipira iliyokufa,” alisema.
Licha ya kutawala mchezo na kuwa na pasi mara mbili zaidi ya Sunderland, Liverpool walishindwa kutengeneza nafasi nyingi za wazi, mpaka Wirtz alipookoa kwa bao la bahati baada ya shuti lake kugeuzwa mwelekeo na beki wa Sunderland.
“Ilifanana sana na mechi ya wikiendi (dhidi ya West Ham), hatukuwa na nafasi nyingi wala hatukubuni nafasi za kutosha kuhakikisha tunashinda, Na bao tulilofungwa leo lilikuwa bahati mbaya mpira umegongwa, ungeweza kwenda kokote lakini ukaenda ndani.” – Slot ameongeza.
Liverpool walinusurika kupoteza kabisa baada ya Wilson Isidor wa Sunderland kujikuta anaenda moja kwa moja kwa Alisson katika dakika za nyongeza, akampita kipa huyo lakini akazuiwa na Federico Chiesa aliyekimbia na kuokoa mpira katika mstari wa goli.




