Kelvin: Ni wakati wangu wa kung’ara Stars

ISMAILIA: MSHAMBULIAJI wa Taifa Stars, Kelvin John, amesema kikosi cha timu ya taifa kipo katika maandalizi mazuri kuelekea mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Kuwait utakaopigwa kesho Ismailia, nchini Misri.
Amesema huu ni wakati wake wa kung’ara tena huku akisisitiza kuwa morali ya wachezaji ipo juu na kila mmoja yupo tayari kuonesha kiwango bora.
Akizungumza mara baada ya mazoezi ya mwisho, Kelvin amesema maandalizi yamekuwa thabiti huku benchi la ufundi likiendelea kutoa maelekezo muhimu kuelekea mchezo huo ambao una umuhimu mkubwa kwa timu inayojiandaa na fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zinazotarajiwa kuanza hivi karibuni.

“Maandalizi yanakwenda vizuri, wachezaji wote wana morali na tuko tayari. Tunaendelea kupokea maelekezo kutoka kwa Mwalimu kuhakikisha tunafanya vizuri,” amesema Kelvin.
Ameeleza kuwa mchezo dhidi ya Kuwait utawapa taswira ya wapi Taifa Stars imesimama kwa sasa na maeneo gani yanahitaji maboresho kabla ya kwenda kushindana kwenye AFCON, ambako Tanzania inatarajiwa kupeperusha bendera yake kwa mara nyingine.
Kelvin, ambaye hajavaa jezi ya Taifa Stars kwa muda mrefu, amesema huu ni wakati wake sahihi kurejea kwa nguvu na kuisaidia timu kupata matokeo, akisisitiza kuwa amejengeka kisaikolojia na kimwili kwa ajili ya majukumu ya taifa.
“Mechi yoyote ya timu ya taifa ni muhimu kwangu. Sijacheza muda mrefu kwenye timu ya taifa, sasa ni wakati wangu kurudi na kufanya ninachokifanya kusaidia timu. Nimejiandaa kisaikolojia na kimwili,” amesema.




