Man City yaweka “Subira” kwenye kesi zao 115

MANCHESTER: MWENYEKITI wa Manchester City, Khaldoon Al Mubarak amesema klabu yake ina “subira” ya kutosha wakati huu ambao klabu hiyo inasubiri hukumu ya kesi yao ya madai ya ukiukaji wa sheria za fedha za Ligi Kuu ya England iliyo katika tume huru ya Mahakama ya michezo nchini humo.
City walipelekwa kwenye tume hiyo mwezi Februari mwaka 2023 kutokana na mashtaka ya ukiukwaji wa sheria hizo za fedha, mashtaka ambayo klabu hiyo imekua ikikanusha vikali. Kesi hiyo ilisikilizwa kati ya Septemba na Desemba mwaka jana lakini bado hakuna uamuzi uliotangazwa.
“Naam, nadhani kitu pekee ninachoweza kusema ni kwamba bado hatuna hukumu, Pindi tu kutakapokuwa na hukumu, nitaweza kuizungumzia. Hadi wakati huo inabidi tuwe na subira, na tutoe muda hukumu itakapokuja tutaizungumzia, nakuahidi, mara tu tutakapokuwa na hukumu.” – Khaldoon alisema katika mahojiano maalum ya kila mwisho wa msimu.
City wanaweza kukabiliwa na adhabu ya kukatwa pointi, kutozwa faini ya mamilioni au hata kushushwa daraja kutoka Premier League hadi Championship iwapo watakutwa na hatia katika kesi hizo zinazozidi100 huku uchunguzi dhidi ya klabu hiyo ukifanywa tangu mwaka 2018.
Mabingwa hao wa msimu uliopita walishtakiwa kwa kukosa kuripoti taarifa sahihi za kifedha kwa misimu tisa kuanzia msimu wa 2009/10 hadi 2017/18, pamoja na kukosa kutoa maelezo kamili ya malipo ya meneja wa zamani Roberto Mancini kati ya msimu wa 2009/10 na 2012/13.
Pia wanashtakiwa kwa kushindwa kutoa maelezo kamili ya malipo katika mikataba ya wachezaji kati ya msimu wa 2010/11 na 2015/16, na kushindwa kutoa ushirikiano wa uchunguzi katika kipindi cha 2018 hadi 2023.
Man City ilishinda Ligi ya Mabingwa mwishoni mwa msimu ambao mashtaka yaliwekwa hadharani, na kujihakikishia nafasi ya kucheza Kombe la Dunia la Klabu lenye timu 32 lililopanuliwa la FIFA ambalo litaanza mwezi ujao.




