Nyumbani

Steve Nyerere awakosoa wanasiasa na viongozi wa dini kuchanganya siasa na mpira/madhabahu

DAR ES SALAAM:MWENYEKITI wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao, Steve Nyerere, amewataka wanasiasa nchini kuacha mara moja tabia ya kuzihusisha timu za Simba na Yanga na masuala ya kisiasa, akisisitiza kuwa jambo hilo linaweza kuchochea migogoro isiyo ya lazima katika tasnia ya michezo nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Steve alisema kuna ongezeko la wanasiasa wanaotumia majina ya klabu hizo maarufu kwa manufaa ya kisiasa, hali ambayo inaleta mgawanyiko usiokuwa wa lazima kwa mashabiki wa soka na taifa kwa ujumla.

“Hizi ni timu kongwe, zimekuwepo kabla hata mimi sijazaliwa. Halafu unakuta mwanasiasa anasema, ‘kama ningekuwa Rais, ningezifuta Simba na Yanga.’ Hii ni hatari kwa mustakabali wa michezo nchini,” alisema Steve Nyerere kwa ukali.

Aidha, Steve hakusita kuwaonya baadhi ya viongozi wa dini ambao wamekuwa wakitumia nyumba za ibada kutoa matamko yenye mrengo wa kisiasa, akisema ni kinyume na maadili ya kiroho na kunahatarisha mshikamano wa kitaifa.

“Kuna mmonyoko mkubwa wa maadili katika jamii, lakini cha kushangaza, viongozi wa dini hawakemei hayo, badala yake wanatumia madhabahu kuzungumzia siasa. Hii siyo sawa na ni hatari kwa amani ya taifa letu,” aliongeza.

Steve Nyerere amesisitiza kuwa ni muhimu kwa taasisi zote – za kisiasa, kidini na kijamii – kushirikiana katika kulinda maadili, mshikamano na amani ya taifa, badala ya kuchochea migawanyiko kupitia majukwaa yasiyo sahihi.

Related Articles

Back to top button