
PEMBA: KOCHA Mkuu wa JKU kutoka Zanzibar, Haji Nuhu, amefichua siri ya ushindi wao dhidi ya Singida Black Stars katika mashindano ya Kombe la Muungano.
Akizungumza baada ya ushindi huo, Nuhu amesema kuwa aliweka mikakati mitatu muhimu iliyomsaidia kuwatoa wapinzani wao waliokuwa na rekodi nzuri ya umiliki wa mpira.
JKU iliibuka mshindi kwa mikwaju ya penati 6-5 kufuatia sare ya mabao 2-2 katika dakika 90 za mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba
Kocha Nuhu amesema mafanikio hayo yalitokana na heshima kwa mpinzani, uchambuzi wa mchezo wao, na ufuatiliaji wa udhaifu wao.
“Unapokutana na timu kubwa lazima uiheshimu, uiangalie vizuri na ujue wapi pa kuwakamata. Nilichunguza jinsi wanavyomiliki mpira na kutafuta namna ya kuwazuia wasitupite kirahisi,” amesema kocha huyo.
Ameongeza kuwa alibaini Singida Black Stars wana uwezo mkubwa wa kumiliki mpira kuliko timu yake, lakini alihakikisha anatumia wakati wanaposhambulia kuipokonya mipira yao na kupunguza makali yao.
Baada ya ushindi huo, JKU sasa inajiandaa kwa hatua ya nusu fainali ambapo itakutana na mshindi kati ya KMKM FC na Azam FC.
Kocha Nuhu amesema wataendelea kufanya maandalizi na kurekebisha makosa yaliyojitokeza kwenye mchezo uliopita ili kuwa imara zaidi.
JKU, timu kutoka visiwani Zanzibar, sasa inaendelea kusaka taji la Kombe la Muungano kwa kujiamini na mbinu madhubuti za kiufundi.