Muziki

BIEN: Bila Size 8 nisingenunua gari

NAIROBI: LICHA ya kuingiza mkwanja mrefu katika maonesho yake mwanamuziki wa Kenya kutoka kundi la Sauti Soul, Bien amefichua kwamba hasingenunua gari kama si ushauri mzuri kutoka kwa msanii mwenzake mwanadada Size 8.

Katika video isiyo na tarehe, Bien, ambaye hivi majuzi alitajwa kuwa Msanii Bora Afrika Mashariki, anaeleza kuwa hakuwa na mpango wa awali wa kununua gari na wala hakujua kuliendesha gari wakati huo.

“Mara ya kwanza niliponunua gari, haikuwa jambo nililopanga. Ni Size 8 ndiye aliyenishawishi kufanya hivyo. Aliniambia, ‘Sasa wewe ni msanii mkubwa, muziki wako unachezwa kwenye redio acha kutumia matatu.’ Yeye ni mtu ninayempenda sana,” akakumbusha.

Pia Bien amefunguka kuhusu ajali iliyobadilisha maisha yake mnamo 2007 ambayo ilimwacha na majeraha mabaya. Wakati akivuka barabara na dadake Biju na wasanii wenzake Wakamba Wawili, Arap Duo, na Wendy Kimani, aligongwa na gari na kusababisha kung’oka kwa meno 16.

“Tulikuwa tumemaliza kurekodi wimbo kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi wakati ajali ilipotokea. Ilikuwa tu kabla ya Wendy kwenda Tusker Project Fame,” alieleza.

Licha ya changamoto alizokumbana nazo, Bien ameibuka na kuwa miongoni mwa wasanii wenye mafanikio makubwa.

Related Articles

Back to top button