Mbadala wa Mbappe apatikana mapema tu

PARIS:PARIS SAINT-GERMAIN (PSG) wamemsajili winga wa Napoli, Khvicha Kvaratskhelia, kwa dau la € milioni 70. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Georgia amesaini mkataba wa hadi Juni 2029 na atavaa jezi namba 7 mgongoni.
Kvaratskhelia alisema: “Ni ndoto kuwa hapa. Ninajivunia kujiunga na klabu kubwa kama hii.” Kvicha anaweza kucheza mechi yake ya kwanza wiki hii dhidi ya Manchester City kwenye Ligi ya Mabingwa.
Rais wa PSG, Nasser Al-Khelaifi, amesema: “Khvicha ni miongoni mwa wachezaji bora na jasiri duniani.”
Akiwa Napoli, Kvaratskhelia alifunga mabao 12 na kusaidia klabu kushinda Serie A msimu wa 2022/23, akishinda tuzo ya MVP wa ligi. Hata hivyo, baada ya kocha Luciano Spalletti kuondoka, Napoli walimaliza nafasi ya 10 msimu uliofuata.
Kocha Antonio Conte, aliyewasili msimu huu, alisema Kvaratskhelia aliomba kuuzwa, jambo lililomshangaza kwani walikuwa wakimtegemea mno.
Anaondoka Napoli akiwa na mabao 30 na asisti 29 katika mechi 107. Aliisaidia pia Georgia kufika hatua ya 16 bora katika Euro 2024.




