Diddy arejea gerezani baada ya kupata jeraha kichwani

NEW JERSEY: Mwanamuziki na mfanyabiashara maarufu wa Marekani, Sean “Diddy” Combs, ameripotiwa kupelekwa kupata matibabu baada ya kupata jeraha kichwani akiwa katika Gereza la FCI Fort Dix, New Jersey na kurejeshwa gerezani.
Kwa mujibu wa taarifa za TMZ, gari la wagonjwa liliondoka gerezani mapema Jumamosi, Oktoba 10, 2026, likiwa limembeba mwanamuziki huyo. Hata hivyo, chanzo cha jeraha hilo na hospitali aliyodaiwa kupelekwa havikufahamika.
Taarifa zinasema Diddy alikuwa na fahamu na alizungumza aliporejeshwa gerezani kabla ya mapambazuko. Msemaji wake alisema timu yake ilikuwa ikithibitisha mazingira ya tukio hilo, huku mamlaka za magereza zikikataa kutoa maelezo kuhusu hali yake ya kiafya.
Diddy anaendelea kutumikia kifungo cha miezi 50 baada ya kupatikana na hatia mwaka 2025 katika makosa mawili yanayohusiana na kusafirisha wanawake kwa madhumuni ya ukahaba. Pia amekata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.
Hadi sasa, hakuna taarifa rasmi ya kina iliyotolewa kuhusu ukali wa jeraha lake au hali yake ya kiafya baada ya tukio hilo.




