Kwingineko

Vega aapa kuwania urais wa FIFA

USWIZI: ALIYEKUWA nahodha wa timu ya taifa ya Uswisi, Ramon Vega, ametangaza dhamira yake ya dhati ya kuwania urais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), akisisitiza kuwa anaingia katika kinyang’anyiro hicho kwa lengo la kushinda na si kushiriki tu.

Vega mwenye umri wa miaka 55 anaamini uzoefu wake wa soka, uwezo wa biashara na uadilifu vitamwezesha kumng’oa madarakani rais wa sasa wa FIFA, Gianni Infantino, katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Machi 2027.

Vega, ambaye aliwahi kucheza kama beki wa kati, alipata umaarufu mkubwa aliposaidia Tottenham Hotspur kutwaa Kombe la Ligi mwaka 1999 licha ya kucheza dakika zote 90 za fainali akiwa na jeraha la kuvunjika kifundo cha mguu. Katika maisha yake ya soka, alicheza zaidi ya mechi 60 za Ligi Kuu England, huku pia akihudumu katika klabu ya Cagliari nchini Italia na Celtic ya Scotland kwa mkopo.

Tangu alipostaafu soka mwaka 2003, Vega amejijengea mafanikio katika sekta ya biashara, huku akitumia uwezo wake wa kuzungumza lugha sita kujenga mahusiano katika maeneo mbalimbali duniani.

Hata hivyo, si mara yake ya kwanza kujaribu kuwania nafasi hiyo ya juu katika soka la dunia, kwani aliwahi kujaribu kuingia kwenye kinyang’anyiro cha urais wa FIFA mwaka 2015, 2019 na 2023 bila mafanikio.

Katika mahojiano na Reuters kupitia Zoom akiwa Dubai, Vega alisema hana shaka na uwezo wake wa kumshinda Infantino wakati vyama 211 wanachama wa FIFA vitakapopiga kura kuamua kiongozi atakayesimamia soka la dunia kwa kipindi cha miaka minne ijayo.

Hata hivyo, ili jina lake lijumuishwe rasmi katika orodha ya wagombea, Vega anatakiwa kupata uungwaji mkono wa angalau vyama vitano vya soka vya kitaifa kabla ya Jumatano ijayo, ambayo ndiyo siku ya mwisho ya kuwasilisha mapendekezo ya wagombea.

Vega alisema hawezi kuingia katika uchaguzi akiwa na mawazo ya kushindwa, akifananisha kampeni yake na mchezo wa fainali aliowahi kucheza akiwa na jeraha. Alisisitiza kuwa yuko tayari kupambana hadi mwisho kwa maslahi ya soka na si kwa manufaa yake binafsi.

Related Articles

Back to top button