Kane kuweka rekodi mpya ya mechi za England

ENGLAND: NAHODHA wa timu ya taifa ya England, Harry Kane, anatarajiwa kuweka historia mpya kwa kuwa mchezaji aliyecheza mechi nyingi zaidi akiwa na jezi ya Three Lions, atakaposhuka dimbani dhidi ya Croatia katika mchezo wa Ligi ya Mataifa utakaofanyika Uwanja wa Wembley, London.
Katika mchezo huo utakaopigwa kesho Alhamis, Kane anatarajiwa kufikisha mechi 126 na kumpiku kipa wa zamani Peter Shilton, anayeshikilia rekodi hiyo tangu mwaka 1990. Hatua hiyo itakuwa mafanikio mengine makubwa kwa mshambuliaji huyo wa Bayern Munich mwenye umri wa miaka 33.
Mbali na rekodi hiyo, Kane ndiye mfungaji bora wa muda wote wa England akiwa na mabao 91. Pia aliwahi kuweka rekodi ya mabao 280 akiwa Tottenham Hotspur kabla ya kujiunga na Bayern Munich mwaka 2023.
Akiwa Ujerumani, Kane ameendelea kung’ara kwa kufunga mabao 156 na kuisaidia Bayern Munich kutwaa mataji ya Bundesliga mwaka 2025 na 2026, huku akitajwa kuwa miongoni mwa washambuliaji wenye ushawishi mkubwa barani Ulaya.
Beki Jarell Quansah wa Bayer Leverkusen amemsifu Kane kwa nidhamu, ubora na uongozi wake, akisema ni mchezaji anayeheshimika Bundesliga na mwenye uwezo mkubwa wa kuamua matokeo ya michezo kupitia mabao yake.
Hata hivyo, pamoja na mafanikio yake binafsi, Kane bado ana ndoto ya kuiongoza England kutwaa taji kubwa la kimataifa, baada ya kupoteza fainali mbili za Euro mwaka 2021 na 2024, akitamani kufuata nyayo za Bobby Moore aliyekuwa nahodha wa England ilipotwaa Kombe la Dunia mwaka 1966.




