Ukitaka kuhudhuria harusi ya Bahati na Diana? andaa milioni 21

NAIROBI: MWANAMUZIKI maarufu kutoka Kenya, Bahati, amezua gumzo baada ya kutangaza mipango ya kufunga ndoa baada ya miaka 10 ya uhusiano wa kimapenzi na Diana.
Lakini kinacholeta mshangao ni gharama kwa anayetaka kuhudhuria sherehe hiyo ambapo anatakiwa kulipa takribani milioni 20.5 hadi 21 za Tanzania ili kupata mwaliko fedha ambazo nis awa na milioni moja za Kenya.
Bahati ameeleza kuwa harusi hiyo itakuwa ya watu wachache, ambapo wageni 100 pekee ndio watakaopata nafasi ya kushiriki katika hafla hiyo inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wake.
“Baada ya miaka 10 ya mapenzi, nimeamua kuufanya uhusiano huu kuwa rasmi. Katika siku hii maalumu, tutakuwa na watu 100 pekee, na yeyote anayetaka kuhudhuria atalazimika kulipa milioni moja za Kenya ili kupata mwaliko,” alisema Bahati.
Kauli hiyo imeibua hisia tofauti miongoni mwa mashabiki, huku wengi wakijiuliza iwapo kiwango hicho cha fedha ni sharti halisi la kupata mwaliko au ni mzaha uliolenga kuvuta hisia za watu kuhusu harusi hiyo.
Iwapo wageni wote 100 watalipa kiasi hicho, jumla ya fedha zitakazokusanywa itafikia KSh milioni 100, jambo linaloifanya kauli hiyo kuvutia zaidi mjadala.
Uamuzi wa Bahati kuweka ukomo wa wageni 100 unaashiria kuwa harusi hiyo itakuwa ya mwaliko maalumu, itakayohusisha idadi ndogo ya watu watakaopata nafasi ya kushiriki katika tukio hilo.
Kwa kawaida, hafla za aina hiyo huhusisha wanafamilia, marafiki wa karibu na watu wengine wenye uhusiano wa pekee na wanandoa. Hata hivyo, Bahati bado hajafafanua namna atakavyounda orodha ya wageni watakaohudhuria.
Mwanamuziki huyo amekuwa akiwashirikisha mashabiki wake katika baadhi ya matukio ya maisha yake binafsi kupitia muziki na mitandao ya kijamii. Hali hiyo inafanya tangazo lake la kutaka kuufanya rasmi uhusiano wake wa miaka 10 kuwa jambo linalovuta hisia za wengi.
Pamoja na tangazo hilo, taarifa muhimu kuhusu harusi hiyo bado hazijawekwa wazi. Miongoni mwa mambo yanayosubiriwa kufahamika ni tarehe ya kufanyika kwa sherehe hiyo, eneo itakapofanyika pamoja na utaratibu wa kupata mwaliko.
Aidha, haijafahamika iwapo malipo ya KSh milioni moja kwa kila mgeni ni sharti rasmi au ni kauli ya mzaha iliyotolewa na mwanamuziki huyo.




