Bundesliga

Xabi Alonso kubaki Bayer Leverkusen

XABI Alonso amesema atabaki katika jukumu lake la ukocha Bayer Leverkusen msimu ujao kwa kuwa anaamini klabu hiyo ni sehemu sahihi kwa kocha kijana.

Alonso amesema hayo leo wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Ujerumani-Bundesliga dhidi ya TSG Hoffenheim Machi 30.

Mhispania huyo amekuwa akihuishwa kwa kiasi kikubwa kuchukua mikoba Liverpool tangu Jurgen Klopp alipotangaza kuachia ngazi mwisho wa msimu.

“Nina hakika ni uamuzi sahihi, nina furaha,” Alonso amesema.

Leverkusen inaelekea kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Ujerumani-Bundelsiga na haijafungwa katika mashindano yote msimu huu.

Alonso amesema wiki iliyopita amewajulisha wakurugenzi wa Leverkusen uamuzi wake wa kubaki klabu hiyo.

Kiungo huyo wa zamani wa Liverpool, 42, pia alikuwa akipewa kipaumbele kuchukua mikoba katika klabu yake nyingine ya zamani Bayern Munich, ambayo kocha wake Thomas Tuchel pia ataondoka mwisho wa msimu.

Alonso alijiunga na Leverkusen mwaka 2022 akitokea Real Sociedad ya Hispania.

 

Related Articles

Back to top button