Odegaard: Kane mbona freshi tu
KITENDO cha Harry Kane kuweka kambani mabao 14 katika michezo 19 ya ‘London Derby’ dhidi ya Arsenal kimemuibua kiungo wa timu hiyo Martin Odegaard akiwataka washika bunduki hao kutomuhofia Mwingereza huyo katika mchezo wa robo fainali Ligi ya Mabingwa usiku wa leo.
Kane amefunga mabao hayo akiwa Tottenham Spurs kabla ya msimu uliopita kujiunga na Bayern Munich ambayo leo itakuwa uwanja wa Emirates katika mchezo wa hatua hiyo.
“Ni mchezaji mzuri, tunajua ubora wake kwenye eneo la hatari, tunapaswa kumheshimu lakini sidhani tunapaswa kuogopa mtu yeyote na tunapaswa kujizingatia sisi wenyewe,” amesema Odegaard.
Kane ni miongoni mwa wafungaji bora Ligi ya Mabingwa msimu huu akiwa na mabao sita katika mechi nane, sawa na Erling Haaland, Kylian Mbappe na Antoine Griezmann.