Tetesi

Mmewasikia hao Azam FC

DAR ES SALAAM: UONGOZI wa Azam FC, umeweka wazi kuwa haujapokea ofa kutoka klabu ya MC Algers ya Algeria kuhusu kuhitaji huduma ya mchezaji wao, Kipre Junior aliyeonyesha uwezo mkubwa ndani ya timu hiyo,

Inasemekana kuwa MC Algers inahitaji huduma ya mchezaji huyo machachari wa waoka mikate hao wa Mbande Dar es salaam na kudaiwa kuwa nyota huyo hatokuwa sehemu ya kikosi cha Azam FC kwa msimu ujao.

Afisa habari wa Azam FC, Zakaria Thabit, ‘Zaka Zakazi’ ameiambia Spotileo hakuna ofa iliyofika kwenye meza yao na wao wanaishia kuona taarifa hizo kwenye mitandao na kama itatokea basi wataweka wazi juu ya maamuzi yao.

Amesema hawauzi mchezaji kwa sababu wanajenga timu imara kwa ajili ya kwenda kufanya vizuri katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, malengo yao ikiwa kucheza hatua ya makundi na kusonga mbele na michuano hiyo.

“Hatuna ofa yoyote na wala mchezaji aliyekuwa sokoni kwa sababu msimu ujao tunaenda kuwakilisha nchini kwenye ligi ya mabingwa Afrika, hatutaki kufanya makosa ya miaka ya nyuma kuondolewa mapema tunahitaji kucheza makundi,” amesema Zaka.

Amesema mipango ya msimu ujao ni kuona timu yao inafanya vizuri katika michuano ya kimataifa pamoja na kuhitaji kutwaa taji la ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya msimu uliopita kufanikiwa kumaliza nafasi ya pili.

Kikosi cha Azam FC kinaingia kambini Julai 4 na 5 mwaka huu kuanza mazoezi rasmi na siku mbili baadae wataenda Visiwani Zanzibar hadi Julai 13 na 14, wataelekea Morocco kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa mashindano.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button