Kakolanya kimeeleweka Namungo

RUANGWA: KLABU ya Namungo FC, ipo katika hatua za mwisho kukamilisha usajili wa aliyekuwa kipa namba moja wa Singida Fountain Gate, Beno Kakolanya ndani ya kikosi hicho kuchukua nafasi ya Deogratius Munishi ‘Dida.’
Namungo, imeamua kuachana na Dida, kwa ajili ya kuimarisha kikosi cha timu hiyo, ambapo inapigania kupata huduma ya Kakolanya, ambaye pia anayehusishwa kutakiwa na Singida Black Stars na Yanga ili kwenda kuchukua nafasi ya Metacha Mnata, anayedaiwa kuwa atatemwa na Mabingwa hao mara 30 wa Ligi Kuu Tanzania bara.
“Ni kweli tunahitaji kuimarisha eneo letu la ulinzi, anaondoka Dida na nafasi yake tunahitaji kumsajili Kakolanya, tunatambua yupo kwenye rada na timu zingine tunapambana ili kufanikiwa kupata huduma yake,” amesema mtoa habari huyo.
Ameongeza kuwa mazungumzo yapo katika hatua nzuri na wanatarajia Kokalanya kuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo kwa msimu ujao akienda kusaidia na Jonathan Nahimana, raia wa Burundi.
“Tunahitaji kuimarisha kikosi cha timu yetu, katika kila nafasi ikiwemo kipa na Kakolanya amepita katika mchakato na tayari mchakato upo katika hatua nzuri na tunatarajia msimu ujao awe sehemu ya Namungo FC,” amesema mtoa habari huyo.
Kipa huyo anadaiwa kuachana na timu yake ya zamani, Singida Fountain Gate, baada ya kuwepo na mgogoro wa kikazi baina yao, hali iliyosababisha kuomba kuondoka ndani ya kikosi hicho.