JKT Tanzania kuendeleza kichapo cha kizalendo
DAR ES SALAAM: Msemaji machachari wa timu ya JKT Tanzania inayoshiriki ligi kuu ya NBC Tanzania bara Masau Bwire amesema timu hiyo haitakuja na kauli mbiu mpya kwa msimu ujao wa 2024/25 badala yake kauli mbiu ya msimu uliopita ya kichapo cha kizalendo (KK) itaendelea.
Masau ameyasema hayo akizungumza kwenye kipindi cha Crown Sports cha Crown FM alipoulizwa iwapo klabu hiyo ya jeshi la kujenga taifa yenye maskani yake Mbweni nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam itakuja na kaulimbiu mpya msimu ujao wa ligi kuu.
“Hatutakuja na jipya, unajua kuna watu wanajiita wananchi, wengine wanajiita wenye nchi lakini sisi ndo wazalendo wenyewe, hatuna mpango wa kubadilika, tunataka uzalendo uendelee” – amesema Masau Bwire.
Katika hatua nyingine Masau amejibu madai ya ushabiki wa timu za Simba na Yanga na kusema kuwa hana ushabiki wala mapenzi na Simba wala Yanga na amekuwa akionesha uungaji mkono wake kwa vilabu hivyo vya Kariakoo vinapokuwa kwenye mashindano ya kimataifa kuiwakilisha nchi.
“Katika hizi timu za kariakoo sina mapenzi na timu yeyote huwa nazisapoti zinapokuwa kwenye michuano ya kimataifa tu, zinawakilisha nchi na kwakuwa mimi ni Mtanzania mzalendo lazima niziunge mkono”
“Hakuna timu yoyote katika hizo ninayoiponda ikiwa inacheza kimataifa au hakuna mtu amewahi kuniona nashabikia timu moja wapo mimi sio shabiki wa simba au Yanga.” amesema