‘Huyu Joshua Mutale akitua kimbieni’
ZAMBIA: KLABU ya Simba ipo katika hatua za mwisho kumsajili winga wa kushoto machachari kutoka klabu ya Power Dyanamos ya Zambia, Joshua Mutale, katika kile kinachoeleza ni kutekeleza alichoagiza Mwekezaji na Rais wa Klabu hiyo, Mohamed Dewji, kuitengeneza timu mpya yenye ushindani na tishio kwa msimu ujao.
Habari kutoka ndani ya Klabu hiyo zinasema kikosi kazi kilichoteuliwa na Mo kwa ajili ya kufanya usajili, kipo Zambia na jana walitarajia kumaliza kila kitu, ikiwemo kupata saini ya mchezaji huyo.
Mutale, Na raia wa Zambia, aliyewachachafya mabeki wa Simba, hasa Shomari Kapombe, katika mechi ya tamasha la Simba Day iliyochezwa Agosti 6, mwaka jana Uwanja wa Benjamin Mkapa, Simba ikishinda mabao 2-0, lakini pia aliwafanya anavyotaka katika mchezo wa raundi ya kwanza, Ligi ya Mabingwa Afrika, Septemba 16 mwaka jana nchini Zambia.
Wakitoka sare ya mabao 2-2, na alikuwa mwiba kwa mara nyingine katika mechi ya marudiano, Oktoba Mosi, mwaka jana, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, zikitoka sare ya bao 1-1, Simba ikitinga hatua ya makundi kwa mabao mengi ya ugenini.
Winga huyo wa Zambia mwenye jezi namba 7 mgongoni, kiwango alichokionyesha kimewashawishi mabosi wa Wekundu hao kuendelea na mawindo yao.
Taarifa zilizopatika kuwa usajili unafanyika kulingana na mapendekezo na mahitaji ya timu hiyo kulingana na nafasi zenye mapungufu baada ya wachezaji sita hadi saba wa kigeni kutemwa.
Amesema hatua hiyo ni kuhakikisha wanaleta wachezaji watakaosaidia timu hiyo kutoka ilipo na kurejea katika makali yake.
“Kama alivyosema Mwenyekiti wa Bodi, Dewji kuwa atafanya usajili mzuri kwa kuleta wachezaji wenye ubora, Mutale miongoni mwa wachezaji waliopo katika mipango yetu na kuna watu wameenda Zambia kwa ajili ya kufanya mazungumzo.
Tutafanya usajili mzuri na kuleta wachezaji watakaokata kiu ya mashabiki na na kuleta kocha mwenye hadhi ambaye ataiondoa Simba hapo ilipo na kurejesha soka letu la ‘Pira Biriani’ limepotea muda mrefu,” amesema Mtoa habari huyo.
Meneja wa Idara ya habari na mwasiliano wa Simba, Ahmed Ally amesema suala la usajili linaenda vizuri na itakapofika muda sahihi wataweka wazi wamewasajili kina nani.
Amewataka wanasimba kuwa watulivu kipindi timu ipo mikononi mwa mwekezaji Mo Dewji kwa kuwapa ushirikiano viongozi kwa kupata utulivu wa kuisuka Simba mpya wanayoitaka.
“Baada ya kipindi kigumu cha mpito sasa tunajenga Simba mpya na imara kusajili wachezaji bora na kuleta matokeo mazuri, ukizingatia Tajiri ameanza kuingia sokoni akisaidiana na timu yake kuangalia aina ya wachezaji kulingana na mapendekezo ya benchi la ufundi,” amesema Ahmed