Nyumbani

Azam FC kutimkia Ufaransa

ZANZIBAR. KIKOSI cha Azam FC, kinatarajia kuweka kambi nchini Ufaransa mapema kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao wa Mashindano yakiwemo Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa ni mara ya pili wanashiriki.

Imeelezwa kuwa hatua ya kwenda nchini humo ni baada ya mapendekezo ya benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha, Youssouph Dabo ambaye anahitaji kupata sehemu tulivu.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo spotileo imezipata, baada ya kukamilika kwa msimu wamepewa mapumziko mafupi na watarejea kambini mapema kwa lengo ya kuhakikisha msimu ujao hawafanyi makosa.

“Ni kweli hatukuwa na msimu mzuri kwa kukosa kutwaa mataji ya ligi ya ndani, lakini tumefanikiwa kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na maandalizi yanaanza mapema ikiwemo mipamgo ya kambi ambayo tutaenda Ufaransa,”.

Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’, wamepoteza mechi ya fainali na wanasahau matokeo hayo na kujipamga kwa msimu mpya wa mashindano.

“Tumemaliza msimu salama, hatukufanikiwa kwa asilimia 100 lakini tumeweza kupata nafasi ya kwenda kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika na maandalizi yanaanza mapema baada ya mapumziko mafupi ambayo watapewa wachezaji.

“Tunatarajia kukutana na kocha, kuona jinsi ya maboresho ya timu yetu ni wachezaji gani ambao tunatakiwa kuwasajili kuimarisha kikosi chenye ushindani kwa msimu ujao,” amesema Popat.

Azam FC jana walishindwa kutwaa taji la kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Yanga kwa mikwaju ya penalti 5-6, baada ya kumaliza dakika 120 bila kufungana, mchezo uliochezwa Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar.

Tangu 2014, Azam FC ilikuwa ikisaka nafasi ya kushiriki ligi ya Mabingwa Afrika lakini ikiwa inajikuta ikiangukia kombe la Shirikisho la Afrika.

Related Articles

Back to top button