Aisha Mnuka ashindwe yeye tu.
DAR ES SALAM: VITA vya ufungaji bora Ligi ya Wanawake Tanzania imekaa pazuri baada ya Kocha wa Simba, Queens, Mussa Hassan ‘Mgosi’, kusema anaimani na mshambuliaji wake Aisha Mnuka kuchukuwa kiatu cha ufungaji bora mwishoni mwa msimu huu.
Amesema licha ya kuendelea na anayomfundisha mazoezini lakini anatumia nafasi ya kumjenga kiakili na kumuondoa presha kwenye mchezo wa mwisho kutakiwa kucheza kwa utulivu.
Mechi ya mwisho ya msimu wa 2023\24, Simba Queens watakabidhiwa ubingwa baada ya ushindi kwenye mchezo dhidi ya Geita Queens, Ijumaa hii uwanja wa Azam Complex, uliopo Chamanzi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Akizungumza na Spotileo, Kocha Mgosi amesema ameendelea kumjenga kisaikolojia na kumnoa zaidi hasa kuelekea mechi ya mwisho kutumia nafasi zinazotengenezwa na kufunga kwa ajili ya kufikia malengo yake.
Amesema hana mashaka na mshambuliaji wake huyo kwa sababu anaimani uwezo wake wa kufunga na matarajio makubwa kiatu cha ufungaji bora msimu huu itakuwa mali yake
“Na asilimia zote Mnuka anakuwa mfungaji bora, kwa sababu naendelea kunoa na kumpa maelekezo katika uwanja wa mazoezi na kwenda kufanya vizuri kwenye mchezo wetu wa mwisho dhidi ya Geita Queens,” amesema Mgosi.
Mnuka anaongoza akiwa na idadi ya mabao 19 anayemfukuzia stumai Abdallah wa JKT Queens akitikisa nyavu mara 18 na kila mmoja amebakiza mechi moja kutamatika kwa Ligi hiyo.